11 Novemba 2019 - 09:00
Cameroon: Uchaguzi wa bunge kufanyika Februari 9

Rais Paul Biya wa Cameroon jana alitangaza kuwa uchaguzi wa bunge utafanyika nchini humo Februari 9 mwakani; katika hatua iliyotajwa na wachambuzi wa mambo kuwa imechukuliwa na Rais huyo ili kuhitimisha mgogoro wa kisiasa wa muda mrefu nchini humo.

(ABNA24.com) Vyama vya upinzani Cameroon kwa upande wake vimepokea kwa tahadhari tangazo hilo la Rais Biya  huku msemaji wa chama kimoja cha upinzani akisisitiza kuwa sheria za uchaguzi zinapasa kufanyiwa marekebisho kabla ya jambo lolote. Uchaguzi wa mwisho wa bunge ulifanyika mwaka 2013 kwa muhula wa miaka mitano; hata hivyo Rais Paul Biya  ambaye amekuwa madarakani Cameroon kwa miaka 37 sasa ameakhirisha mara mbili uchaguzi mpya.

Biya alichaguliwa kuiongoza tena Cameroon mwaka uliopita hata hivyo matokeo ya uchaguzi huo wa Rais yalipingwa na mpinzani wake mkuu Maurice Kamto wa chama cha MRA. Kamto mwenye umri wa miaka 65 alifungwa jela mwezi Januari mwaka huu na kuachiwa huru mwezi Oktoba baada ya chama chake kufanya maandamano kadhaa ya kupinga matokeo yaliyompa ushindi Rais Paul Biya.

Cameroon imekuwa ikihesabiwa kama nchi yenye utulivu wa kiwango fulani kwa miaka kadhaa sasa licha ya kuathiriwa na mapambano ya miaka miwili ya wanaotaka kujitenga upande wa magharibi mwa nchi hiyo sambamba na kujiri mashambulizi ya kundi la kigaidi la Boko Haram.

..........
340